UJENZI WA BANDA LA KUKU


Ujenzi wa mabanda bora ya kuku ni miongoni mwa mambo ya msingi kabisa katika ufugaji bora wa kuku wawe ni wa asili au wale walioboreshwa. Hata hivyo si kila mtindo wa ujenzi unafaa, kwahiyo ujenzi huo ni lazima uzingatie mahitaji halisi ili ufugaji huo uweze kutoa matokeo bora yanayotarajiwa na mfugaji.
Mambo muhimu katika ujenzi wa banda la kuku ni;

1. Liingize hewa safi wakati wote.
2. Liwe kavu daima.
3. Liwe nafasi ya kutosha.
4. Liwe la gharama nafuu lakini la kudumu.
5. Lizuie kuingia wanyama na wadudu hatari kwa kuku.
6. Liwe na nafasi ya kuweka vyombo vya chakula na maji.
7. Lizuie upepo wakati wa baridi kali.


HEWA NA MWANGA:

Hewa ni muhimu kwa kila kiumbe, hivyo banda la kuku ni lazima liingize hewa safi na kutoa ile chafu na liweze kuingiza mwanga wa kutosha

1. Kwa kifupi ni kwamba madirisha ya banda ni lazima yawe makubwa na ya kutosha ili yaingize hewa safi na kutoa ile chafu.
2. Ni vema madirisha haya yawe juu kiasi cha meta moja (1) kutoka chini ili hewa ipite juu ya vichwa vya kuku.
3. Hewa safi siyo upepo, hivyo jaribu kuzuia upepo mkali kuingia ndani ya banda la kuku ama sivyo kuku wataugua ugonjwa wa mafua na niumonia na vifaranga vinaweza kufa kwa ugonjwa wa baridi.
4. Jenga Banda lako kwa kukinga upepo unakotokea na kupanda miti kuzunguka banda hilo la kuku ili kupunguza kasi ya upepo na kuweka kivuli dhidi ya jua kali na joto.


UKAVU NA USAFI WA NDANI:

Kwa vile kuku si ndege wa majini kama bata , ni jambo la busara kuhakikisha kuwa mahali anapoishi hapana unyevunyevu.

1. Banda la kuku lijengwe mahali palipoinuka ili kuzuia maji ya mvua yasiingie.
2. Wajengee kuku uchaga wa kulalia kwa kuweka viguzo vyenye urefu wa meta moja na kutandika miti juu yake ili usiku walale hapo, kuliko kuwalaza ardhini au sakafuni.
3. Ukavu wa banda ni muhimu sana hasa kwa vifaranga na kuku wanaotaga. Ndani ya banda lenye unyevu mayai kuchafuka sana hata wakati mwingine huoza kwa urahisi na jitihada zako zitakuwa ni bure.
4. Sakafu ya banda ni vizuri ikawa ya zege lakini kutokana na uhaba wa fedha sakafu inaweza kutengenezwa kwa mabanzi (mabanda yaliyoinuliwa) au udongo mgumu na au mchanga ambao utafunikwa kwa mabaki ya taka za mpunga na yale ya mbao.
5. Ili kuepuka unyevunyevu ni vyema eneo/mahali pla kujenga banda pawe pameinuka na penye kupitisha hewa ya kutosha.


PAA LA BANDA:

Paa la banda liwe madhubuti ili kuzuia maji ya mvua kuingia hasa wakati wa masika. Sakafu ya banda iwe juu zaidi ya usawa wa nje. Paa linaweza kuezekwa kwa mabaki ya vipande vya bati , madebe na kama ikishindikana tumia nyasi zinazofaa kwa ajili ya kuezeka nyumba katika eneo hilo.


NAFASI YA KUFANYA KAZI:

Banda la kuku lisiwe na nguzo au mbao nyingi sana ndani kiasi cha kumfanya mhudumiaji wa kuku ashindwe kufanya kazi zake. Hali hiyo itamfanya apoteze muda mwingi katika kuzizunguka nguzo hizo, hasa wakati wa kuokota mayai au kufanya usafi.


VIFAA:

Unapotaka kujenga banda la kuku kwanza kabisa tayarisha vifaa vinavyotakiwa. Vitu kama miti au nyasi, nyavu au fito, misumari au kamba ni muhimu kuviandaa mapema.

Pili ni lazima uwe na plani/ramani kamili ya banda hilo. Kwa wastani kila kuku anahitaji nafasi ya Meta za eneo la 0.11 hadi 0.22 (futi 1 hadi 2 za eneo.) kutegemeana na umri wa kuku.

UJENZI RAHISI:

Kuku wafugwao hatimaye ni lazima wafidie gharama za Ujenzi wa mabanda na chakula. Gharama zikiwa kubwa sana huenda ukaifanya shughuli ya ufugaji isiwe na faida hata kidogo hali hiyo itamfanya mfugaji aone ufugaji hauna maana yoyote kwake. Lakini ukijenga banda lako kwa kutumia vifaa vinavyopatikana kwa urahisi utaongeza faida zaidi kwakuwa umepunguza gharama za uendeshaji wa mradi.


VIPIMO:

Banda la kuku linatakiwa liwe na Meta 15 hadi meta 22 za eneo yaani Meta 3 hadi 4.5 za upana kwa meta 5 za urefu. Banda hili linaweza kutunza kuku 100 wakubwa kwa wakati mmoja.


HITIMISHO;

  • Ujenzi wa mabanda unasisitizwa katika kuboresha ufugaji wa kuku wa asili ili;
  • Kuongeza uzalishaji na kupunguza vifo vya vifaranga kwa majanga mbalimbali kama vicheche ,mwewe, mapaka, mbwa na wizi wa kuku wanaozurura holela.
  • Vile vile inatarajiwa kwamba kuku wanaozuiliwa kwenye banda na kuwekewa chakula mchanganyiko wataongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa.

Kilimo bora cha Dengu


UTANGULIZI
Dengu ni zao la chakula na biashara lenye kiasi kikubwa cha protini, vitamini A na B, Madini ya Potassium na chuma. 
Zao hili likilimwa vizuri linaweza kutoa mavuno ya kilogram 200 hadi 500 kwa ekari.Zao hili huchukua wastani wa siku 135 kupandwa hadi kuvunwa.

HALI YA HEWA NA UDONGO
Ni zao linalohitaji hali ya hewa ya kibaridi kiasi kwani joto kali na ukame sana huathiri mavuno yake,hupunguza wingi wa mavuno. 
Ni zao linalostahimili ukame,linaweza kukua katika hali ya hewa ya unyevunyevu tu.Kama utakuwa unamwagilia basi epusha unyevu mwingi ikifikia kipindi cha maua hadi kuvuna.Zao hili linaweza kulimwa katika udongo wa aina tofauti tofauti wenye P.H 6-8.Udongo wenye asidi na base kidogo.Kwa Tanzania zao hili linaweza kulimwa katika mikoa ya Iringa,Dodoma,Mwanza,Singida,Morogoro N.K 

UPANDAJI NA NAFASI
Zao hili huitaji mbegu kiasi cha kilogram 15 hadi 40 kutegemea ukubwa wa mbegu husika. 
Zao hili hupandwa mwishoni mwa msimu wa mvua,unaweza kupanda baada ya kuvuna mazao mengine uliyopanda mapema, 
Mbegu za dengu hufukiwa katika kina cha sentimeta 4 hadi 6 ili kufanya mazingira rafiki kwa bacteria wa rhizobia kufanya kazi.Zao hili usipande pamoja na vitunguu na tangawizi.Panda kwa kutumia drilling method-njia ya vifereji kwa nafasi ya mistari miwili ya sentimeta 15 na sentimeta 30 hadi 50 kwa mstari hadi mstari.

MBOLEA ZA VIWANDANI NA SAMADI
Mbegu unaweza kuzipanda baada ya kuziongeza inoculam kundi F na Pia Mbolea ya DAP kilogram 25 hadi 50 kwa ekari katika shamba lisilo na rutuba ya kutosha.

PALIZI-Palilia mapema shamba lako.

WADUDU WAHARIBIFU KWA DENGU
Dengu hushambuliwa na Mchwa wakubwa weusi,aphid wa njegere,funza wa vitumba,Inzi wa lucina n.k
wazuie wadudu hawa kwa kupuliza dawa za wadudu mara tu uonapo dalili za mashambulizi ya wadudu.

MAGONJWA YA DENGU
Dengu hushambuliwa sana na magonjwa ya ukungu ambayo.Hivyo kama eneo lako hushambuliwa na ukungu mara kwa mara basi puliza dawa za ukungu (FUNGICIDES)


UVUNAJI WA DENGU
Zinavunwa mara tuu pindi vitumba vya chini vibadilikapo rangi kuwa kahawia angavu na vitumba vikiguswa hutoa sauti.

KILIMO BORA CHA CHOROKO MUNG BEAN ( Vigna radiata)


UTANGULIZI

Choroko ni zao la chakula na biashara lenye kiasi kikubwa cha protini na madini ya phosphorus na calicium.Zao hili likilimwa vizuri hutoa mavuno kati ya Kg 400 hadi 900 kwa ekari.

UDONGO NA HALI YA HEWA IFAAYO.
Choroko hustawi katika udongo wa aina tofauti tofauti usiotuamisha maji.Hulimwa kutoka mita 0 hadi 1500 kutoka usawa wa bahari japokuwa kuna mbegu nyingine zinaweza kukubali zaidi ya ukanda huu.Hili ni zao linalostahimili ukame.

AINA ZA CHOROKO
Kuna aina kuu mbili za choroko ambazo pia zimegawanyika katika makundi mawili,choroko nyeusi na choroko za kijani.
1. CHOROKO ZINAZOTAMBAA-hizi ni choroko ambazo zinarefuka sana na hutambaa sehemu mbalimbali.
2. CHOROKO ZINAZOSIMAA=Hizi ni choroko ambazo zinakuwa kwa kusima kwenda juu.Hizi huchukua muda mfupi kukomaa wastani wa siku 60-70

KIPINDI KIZURI CHA UPANDAJI WA CHOROKO
Choroko hazihitaji maji mengi hivyo ni budi zipandwe mwishoni mwa msimu wa mvua,Pia zinaweza kupandwa katika shamba lililolimwa mpunga.

NAFASI ZA UPANDAJI WA CHOROKO NA KIASI CHA MBEGU
Choroko huitaji mbegu kiasi cha kilogram 8 hadi kumi kwa ekari moja.
Panda choroko zako kwa nafasi ya sentimeta 30 mastari na mstari na sentimeta 10 shina hadi shina (30 x10 )sentimeta au (40 x 8 )sentimeta

SAMADI NA MBOLEA ZA VIWANDANI
Kama shmba lako halina rutuba ya kutosha unaweza kuongeza samadi kiasi cha tani tano kwa ekari na pia unaweza kupanda kwa kutumia mbolea ya NPK kg 50 kwa ekari.weka mbolea zote kabla ya kupanda.
www.kilimofaida.blogspot.com
UMWAGILIAJI
Kama umepanda kipindi cha ukame sana au unalima kilimo cha umwagiliaji basi mwagilia shamba lako upate unyevu wa kuotesha mbegu, kisha baada ya mbegu kuota kaa siku 6 hadi 10 na umawgilie tena. Mara tatu za kumwagilia zinatosha kwa choroko.

PALIZI
Palilia shamba lako mapema kuzuia magugu.Palizi moja inaweza kutosha.

MAGONJWA YA CHOROKO

1-yellow mosaic virus ( Ugonjwa wa manjano)
Dalili- mmea unakuwa wa njano na madoa ya njano katika majani.
Kinga na tiba-Panda mbegu zinazostahimili magonjwa.









2-Powdery Mildew (Ukungu)
Dalili-Majani yanakuwa na vidoti vya njano ambavyo vinabadilika kuwa vya kahawia au kijivu haraka na ambapo kunakuwa na unga unga katika majani.
Kinga na tiba-Panda mbegu zinazostahimili ukungu,Pulizia dawa za ukungu (Fungicide).
anza kupuliza wiki tatu baada ya mimea kuota na kuendelea kulingana na hali halisi.




3 LEAF SPOT (Vidoti katika majani)
Dalili-majani yanakuwa na vidoti vya mviringo na visivyo na umbo maalum ambapo katikati yanakuwa na rangi rangi ya kijivu na weupe na mistari ya rangi ya wekundu-kahawia au nyeusi-kahawia.ugonjwa huu husababisha hasara hadi ya asilimia 58 ya mapato.
Kinga na Tiba-Panda mbegu inayostahimili ugonjwa huu,Choma mabaki ya mimea hii na ile ya jamii moja baada ya kuvuna.Pulizia dawa za ukungu (Fungicide) Katika nafasi ya wiki mbili mbili kama eneo hilom linashambuliwa mara kwa mara na ukungu.











WADUDU.
Kuna wadudu mbalimbali wanaoshambulia choroko kama vile aphidi,funza wa vitumba,nzi wa maharage.Wazui wadudu hawa kwa kupuliza dawa za wadudu mara tu baada ya mimea kuota,dawa kama karate,twigathoate,dimethote na nyinginezo zinaweza kutumika.

UVUNAJI

Mara tuu choroko zinapofikia asilimia 85 ya ukaukaji zinabidi zivunwe ukichelewa zitapukutikia shambani.

Ufanisi na Kilimo bora cha Ufuta

UFUTA (Sesamum indicum)

UTANGULIZI
Ufuta (simsim/sesame) ni zao la kibiashara ambalo mbegu zake zina kiasi kikubwa cha mafuta kiasi cha asilimia 45 hadi 55.Na zao hili linaweza kulimwa maeneo mengi ya Afrika mashariki na Tanzania.Ni zao ambalo linatowa mafuta yenye thamani kubwa na hivyo kulifanya zao bora la biashara.

HALI YA HEWA INAYOFAA KWA KILIMO CHA UFUTA

Zao hili linawezwa kulimwa katika maeneo yanayopata mvua kidogo.Maeneo ya ukanda wa chini usawa wa bahari hufaa zaidi kwa kilimo cha ufuta.Pia nyanda za juu ambazo ni chini ya mita 1500 hufaa kwa kilimo cha ufuta.Mfano kwa Tanzania unaweza Ukalima ufuta katika mikoa ya Morogoro,Lindi,Manyara,Dodoma,Iringa.


UDONGO UNAOFAA KWA KILIMO CHA UFUTA

Ufuta ustawi vizuri katika maeneo yenye udongo mwepesi mweusi na usiotuamisha maji,udongo tifutifu ni mzuri kwa kilimo cha ufuta,Pia ufuta unawezwa kulimwa katika udongo wowote lakini usiotuamisha maji.Ufuta hufa haraka kama maji yatatuama kwa muda mrefu shambani.

AINA ZA UFUTA

Kuna aina kuu mbili za mbegu za ufuta:

1) MBEGU ZA ASILI
Wakulima wengi hupanda mbegu za asili, mbegu ambazo zilianza kulimwa miaka mingi iliyopita.Mbegu hizi nyingi zina mavuno kidogo na huchukua muda mrefu kukomaa Huchukua siku 140 hadi 180.

2) MBEGU ZA KISASA
Mbegu hizi zinakomaa kwa muda mfupi na hutowa mavuno mengi, wastani wa kilogram 500 hadi 800 kwa ekari kama shamba litaandaliwa litapandwa na litatunzwa vizuri.Mbegu hizi huchukua siku 105 hadi 140 kukomaa.Mfano wa mbegu hizi ni Naliendele 92,Lindi 202,Ziada 94 na Mtwara 2009.

UPANDAJI WA UFUTA

Shamba la ufuta ni budi likatuliwe na kulimwa vizuri kabla ya kupanda,hata hivyo pia unaweza kupanda bila kukatua lakini mavuno yatapungua kidogo.Inashauriwa kupanda ufuta kwa mistari kwa vipimo vifuatavyo.Sentimeta 50 kwa 10 au 50 kwa 20 kama utapanda kwa kutumia mistari ya kuchimba vijifereji vidogo katika mstari na kudondosha mbegu hizo katika vifereji hivyo (Drilling method) na kwa kuacha mche mmoja mmoja kwa kila shina.
Pia sentimeta 50 kwa 30 au 60 kwa 30 kwa kuacha miwili kwa kila shina. Kwa Mbegu ya Asili Unaweza Kupanda kwa sentimeta 70 kwa 30 kwa Kuacha Miwili kwa Kila shimo.Fukia mbegu kwa sentimenta .2.5 hadi 5.

MUDA WA KUPANDA

Muda mzuri wa kupanda ufuta ni mwanzoni mwa msimu wa kilimo yaani Mwishoni mwa mwezi Desemba hadi katikati kwa mwezi Januari.

MATUMIZI YA MBOLEA

Ufuta ni zao ambalo halihitaji matumizi makubwa ya Mbolea.Japokuwa hustawi zaidi katika udongo wenye rutuba ya kutosha.Kama utapanda katika ardhi isiyo na rutuba ya kutosha basi unaweza kutumia mbolea kiasi kidogo Mbolea kama vile UREA na BUSTA.

MATUNZO NA PALIZI

Miche ya ufuta ni midogo na laini sana hivyo inahitaji palizi mapema hasa katika kipindi cha majuma manne ya kwanza .Pia katika kipindi hiki unatakiwa kupunguza miche iliyosongamana.Kadri utavyochelewesha palizi na kupunguzia mimea mapema ndivyo unavyoifanya mimea isikuwe vizuri na kujipunguzia kipato chako.

MAGONJWA YA UFUTA

Magonjwa makuu ya ufuta ni madoa ya majani na kuoza matawi na shina.Zuia magonjwa haya kwa Kupanda mbegu bora na kwa kutokupanda ufuta katika ardhi inayotuamisha maji,pia itawezekana kubadilisha shamba usilime ufuta katika shamba lililolimwa msimu uliopita.


WADUDU WANAOSHAMBULIA UFUTA

Kuna wadudu wengi wanaoshambulia ufuta kama vile vibaruti (Ambao hushambulia hatua ya mwanzo kabisa ya miche iliyoota ya ufuta ambapo vibaruti hula majani ya mwanzo ya mmea mara tu yanapojitokeza).Pia Aphidi hushambulia ufuta kwa kufyonza maji katika majani ya mimea hivyo kupelekea kukauka kwa majani ya mmea.
Pia wapo funza wa majani ambao hula majani ya mimea na pia hufunga majani ya ncha ya mimea na kuzuia ukuaji wa matawi wa mimea,wadudu hawa ni hatari zaidi kwani wanazuia kutengenezwa kwa vitumba vya ufuta.
Kuzuia vibaruti,kabla hujapanda mbegu yako changanya na dawa ya tunza au gaucho.Pia panda mbegu bora na fanya mzunguko mazao shambani.Wadudu wengine wakijitokeza tumia dawa kama karate,dimethoate.Twigathoate,duduall,duduba na dawa nyingine za wadudu kabla wadudu hawajasababisha madhara makubwa shambani.

UVUNAJI

Ufuta uliokomaa tayari kwa kuvunwa utaonesha mabadiliko ya majani yake na shina na matawi yatabadilika rangi yake na kuwa njano au kahawia au yataanza kukauka,pia vitumba vya mwanzo vitaanza kubadilika rangi yake na kuanza kukauka hivyo utatakiwa ukate ufuta mapema kabla vitumba havijakauka na kupasuka.Vuna ufuta wako kwa kukata matawi ya ufuta na kuyafunga katika matita ya saizi inayokufaa ila yasiwe matita makubwa sana ambayo hayatakauka katikati kwa urahisi yasimamishe matita yako kuelekeza juu kisha acha yakauke kwa wiki mbili hadi nne kutegemea na ukali wa jua.vitumba vikisha kauka na kupasuka tandika mkeka au turubai na yageuze matita yako katika mkeka na turubai hapo ufuta utamwagikia katika mkeka au turubai lako,kuupata ufuta unaokwama katika matita piga piga kidogo tita unapoligeuza.Kisha Peta ufuta wako na kuuweka katika Vyombo safi vya kuhifadhia.

Kilimo Cha Mbaazi Tanzania


Mbaazi ni moja kati ya mazao yanayo limwa kwa wingi nchini Tanzania 
Hali ya hewa  inafaa kwa kilimo kwa kilimo mbaazi ni nyuzi joto 18 hadi 38sentigredi.mbaazi huwa hazivumialii barafu .Mbaazi hustawi kwenye mvua kwa mwaka kiasi cha milimita 600 hadi 1000 inagawa aina za muda mfupi hustawi kwenye kiwango kidogo cha mvua milimita 250.hazistawi zaidi kwenye usawa wa bahari
AINA ZA MBAAZI
Kuna makundi makuu matatu ya zao la mbaazi

MBAAZI ZA MUDA MREFU


Huchukua miezi sita mpaka saba shambani mpaka wakati wa kuvuna.
Zina matawi machache na ni ndefu hvyo hufaa sana kwa kilimo mseto.haini zinaweza kuvunwa zaidi ya msimu mmoja lakini mazao yanayopatikana baada ya msimu wa kwanza huwa madogo hivyo inashauriwa aina zipandwe upya kila mwaka
USTWAI;Aina hizi hustawi vizuri katika ukanda wa juu na kati wenye mvua za kutosha .

MBAAZI ZA MUDA WA KATI

SIFA ZAKE
Hukomaa ndani ya muda wa miezi minne na nusu mpaka miezi sita baada ya kupandwa.zina matawi mengi na ni fup kulingana na mbaazi za muda mrefu.hazikomai zote kwa wakati mmoja humlazimu mzalishaji kuvuna zaidi ya mara moja ingawa mazao ya kwanza ni mengi kuliko mazao yanayofata.zinapendwa na kina mama kwa sababu ya mboga kwa jili ya mboga au enderefu kwa sababu huchanua tena mara zikipata maji
USTAWI;Aina hii ya mbaazi hulimwa katika ukanda wa kati mita 800 hadi 1100 usawa wa bahari zenye mvua za wastani

MBAAZI ZA MUDA MFUPI
Kundi hili linawakilisha aina bora za mbaazi za muda mfupi yaani miezi 3 hadi 3 na nusu.


SIFA ZAKE

Aina hii ni fupi ni mita moja hadi moja na nusu yenye mauwa mekundu inapoanza kuchanua hulimwa katika ukanda wa kati na wa chini katika uhaba wa mvua kama vile maeneo ya pwani
Aina hii hazichanganywi na mahindi ,inahatari ya kushambuliwa sana na wadudu hasa ukanda wa kati na wa juu sababu huchanua wakati wa mvua
Tofauti na aina zote za mbaazi aina hii haiasiliwi nan a urefu au ufupi wa siku hivyo itachanua wakati wowote mara baada tu ya kupanda
Haina hii ya mbaazi haina ukinzani wa ugonjwa wa kunyauka

MATUMIZI YA MBAAZI
Chakula kwa binadamu
Kilimo cha mseto,mbaazi za muda wa kati na muda mrefu zinaweza kulimwa mseto na mzao mengine ya jamii ya nafaka mfano mahindi , mtama ,uwere
FAIDA ZA KULIMA MBAAZI NA MAZAO MENGINE
1 Matumizi bora ya ardhi hasa kwa kuwa mbaazi huongeza ufyonzaji wa hewa ya naitrogen shambani
2 Mzalishaji atapata mazao mawili au zaidi katika shamba mojana msimu mmoja
3 Kipato cha mzalishaji kitaongezeka kutokana na mazao mengine
4 Pia mafuno ya mazao ya nafaka kama mahindi hayapungui kwa kiasi kikubwa kutokana na mchango huo wa mazao

UTAYARISHAJI WA SHAMBA
1 N’goa visiki pamoja na mabaki yote ya mimea kabla ya uzalishaji
2 Lainisha udongo kwa kupiga halo mbaazi zinavyoota huwa dhaifu sana na kama shamba halikuandaliwa vizuri magugu huota mapema kabla ya mbegu za mbaazi
3 Tayarisha matuta au makinga maji kama shamba lipo kwenye mteremko .



KUANDAA MBEGU
Mbegu bora iliyochaguliwa vizuri na kuhakikiwa kiwango cha uwotaji iandaliwe
 Mbegu ziwekwe dawa za kuzuia kuvu kabla ya kupanda ili kuzuia magonjwa yatokanayo na mbegu na udongo
MBEGU BORA
Mbegu za mbaazi zimegawanywa kwenye makundi makuu matatu
1 mbegu ya mda mfupi
2 mbegu ya mda wa kati
3 mbegu ya mda mrefu
UOTESHAJI
Nafasi kutoka mstari hadi mstari hutegemea zao kuu linalopandwa .kilimo mseto na mahindi hutegemeana pia na aina za mbegu sentimita 90 mpaka 120 sentimita unashauliwa kutoka mstari hadi msatri 50 sm kutoka shimo hadi shimo acha mimea miwili kwa shimo
Panda mahindi yanayo komaa mapema ili yavunwe mapema na kutoa nafasi kwa mbaazi ili kuchanua na kutanuka
Tumia kilo 4 hadi 5 kwa hekari kutegemeana na ukubwa wa punje
 UPANDAJI
Mbaazi za mda mrefu panda kwa mistari kwa umbali wa sm150 kwa sm100
Mbaazi za muda wa kati panda kwa mstari wa sm100 kwa 60sentimita
Mbaazi panda kwa umbali wa nafasi sm90kwa 60sentimita
MBOLEA
Mbaazi hustawi vizuri kwenye shamba lenye mbolea ya kutosha.Hivyo inapendekezwa kwamba kila mzalishaji aweke mbolea ya samadi ili kuhifadhi arhdi dhidi ya upotevu mkubwa wa mbolea
Jamii ya mikunde hujitengenezea aina ya mbolea ya naitrogen . hata hivyo tafiti zinaonesha kwamba matumizi ya mbolea za kupandia kama mabolea ya minjigu ,TSP,OAP,kutaimarisha mizizi na mshina na hivi kuongeza uzalishaji

PALIZI NA KUPUNGUZA MIMEA
Ni muhimu kuoalilia mapema kuondoa magugu ambayo hushindana na mimea .palizi ifanyike mara mbili kwa wakati.palizi tatu inategemea wingi wa majani na unyevu au mvua . mishe ikiwa mingi kwenye shina husabsbisha mazao kidogo kutokana na mimea kushindania mwanga na virutubisho. Palizi inaweza kufanyika kwa jembe la mkono au trector kulingana na nafasi iliyotumika katika kupanda . palizi mbili za mwanzo kati ya siku 60 za mwanzo ni muhimu kbla ya mbaazi hazijawa na kivuli cha magugu kumea lakini pia kiuwa gugu kinaweza kutumika kabla ya mbaazi kuota .baada ya mbaazi kuota dhidi ya magugu ya majani mapana ichanganywe Fluazifopbutyl kudhibiti magugu jamii ya nyasi,kiuwa gugu kitumike wakati mbaazi zimekua kufikia sentimita 25 hadi 30 .Nimuhimu kupunguzia miche na kubakiza miwili au kutegemeana na nafasi iliyo tumika
  
UVUNAJI WA MBAAZI
Mbaazi zikisha komaa na kuanza kukauka zivunwe mapema kwa kukatwa matawi yenye mbaazi na kukausha zaidi kisha mbaazi zitenganishe kwa mikono au kwa kupigwa hayo mati taratibu baada ya kukaushwa sana

Kilimo Bora cha zao la Karanga

Karanga ni mojawapo ya mazao yanayotoa mafuta. Katika Tanzania zao hili hustawi zaid katika mikoa ya Kusini Mashariki, Dodoma na Morogoro. Pamoja na kutoa mafuta vile vile zao hutumika kwa njia nyingine mbali mbali, nazo ni pamoja na:


1. Chakula cha wanyama (Mashudu na majani)
2. Kurutubisha ardhi
3. Chakula cha binadamu (Confectionary)

Kwa ujumla zao hili hutumika na wakulima kama zao la biashara.



HALI YA HEWA
Karanga hustawi vizuri katika maeneo yaliyopo kwenye miinuko chini ya mita 1500, toka usawa wa bahari katika Tanzania, na hustawi zaidi katika maeneo ambayo yanapata mvua za wastani wa mm 750hadi mm 1200 kwa mwaka.
Vile vile karanga hustawi vizuri kwenye udongo wa kichanga, inashauriwa kutopanda karanga kwenye udongo mzito (mfinyanzi) hii ni kutokana na sababu kwamba, karanga hazistawi kwenye sehemu zinazo simama maji, na udongo mzito huleta hasara wakati wa uvunaji.

AINA ZA KARANGA
Kuna aina kuu tano bora za karanga ambazo zimetolewa kwa wakulima hapa nchini.

a. Red Mwitunde 
Ilitolewa kwa wakulima miaka ya 1950.
Mbegu za muda mrefu (Virginia Spreading bunches). 
Huchukua muda wa siku 120 -140 toka kupanda hadi kukomaa. Ina uwezo wa kutoa kilo 1000 kwa hekta. Mbegu zake ni kubwa na zina rangi nyekundu. 

b. Nyota
Ilitolewa mwaka 1983.
Mbegu ya muda mfupi ( Spanish Errect Banch). 
Huchukua siku 90-100 tangu kupanda hadi kukomaa. Ina uwezo wa kuzaa wastani wa kilo 1500 kwa hekta. Mbegu zake ni ndogo, na zina rangi ya udongo (Tan).
Aina hii ya mbegu zina tabia ya kuanza kuota tena shambani mara tu zikiisha komaa, hivyo ni muhimu kuzivuna mapema zikisha komaa.

c. Johari:
Ilitolewa mwaka 1985.
Mbegu ya muda wa kati (Virginia Spreading Bunches).
Huchukua siku 110 - 120 toka kupanga kuvuna. Mbegu zake ni kubwa na zina rangi ya udongo (Tan). Ina uwezo wa kutoa wastani wa kilo 1000 kwa hekta moja. 

d. Pendo: . 
Ilitolewa mwaka 1998.
Mbegu ya muda mfupi ( Spanish Errect Banch). Huchukua siku 90-100 tangu kupanda hadi kukomaa. Ina uwezo wa kuzaa wastani wa kilo 1500 kwa hekta. Maganda yake ni laini na mbegu zake ni kubwa, na zina rangi ya udongo (Tan). Kama Nyota, aina hii ya mbegu ina tabia ya kuanza kuota tena shambani mara tu zikisha komaa, hivyo ni muhimu kuzivuna mapema zikisha komaa.

e. Sawia:
Ilitolewa mwaka 1998.
Mbegu ya muda wa kati (Virginia Spreading Bunches).
Huchukua siku 110 - 120 toka kupanga kuvuna. Mbegu zake ni kubwa na zina rangi ya udongo (Tan). Ina uwezo wa kutoa wastani wa kilo 1000 kwa hekta moja. 

Pamoja na mbegu zilizotajwa, kuna aina nyingine nyingi za kienyeji (local varieties) zinazotumiwa na wakulima katika sehemu mbali mbali.
UTAYARISHAJI WA SHAMBA
Shamba litayarishwe vizuri kuwezesha udongo kupenyesha maji na mizizi kirahisi. Karanga hupandwa kwenye matuta au sensa (shamba tambarare).

UTAYARISHAJI WA MBEGU
Karanga ambazo zinakusudiwa kwa mbegu zitunzwe na maganda yake bila kubanguliwa. Zibanguliwe karibu na msimu wa kupanda na kuchaguliwa. Baada ya kuchaguliwa zitiwe dawa, aina ya Fernasan D, Katika uwiano wa gramu 28 za dawa kwa kila kilo 10 za mbegu safi.
WAKATI WA UPANDAJI
Uamuzi wa kuchagua wakati mzuri wa kupanda niule utakaoliwezesha zao hilo kukomaa wakati wa mvua za mwisho. Kuchelewa kupanda, hupunguza mavuno. Ni muhimu kuchagua aina ya mbegu ambazo uvunaji wake unafanana na mazingiza ya eneo hilo kihali ya hewa.
Kwa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, karanga za muda wa kati na mrefu (Johari, Red Mwitunde) zipandwe kuanzia katikati, hadi mwishoni mwa mwezi Desemba. Karanga za muda mfupi(Spanish na Valencia) zipandwe kuanzia mwishoni mwa mwezi Desemba hadi katikati ya mwezi Januari.
Kwa mikoa ya Tanga, Morogoro na sehemu za mkoa wa Dodoma, karanga zipandwe mapema mwanzo wa mvua ndefu. (Februari/March).

NAFASI KATI YA MIMEA
Inashauriwa kupanda karanga katika mistari. Nafasi kati ya mistari ni sentimita 50, na kati ya mimea ni sentimita 15, kwa karanga zinazotambaa (Virginia Spreading types). Kama karanga zinapandwa kwenye matuta ya sentimita 90, zipandwe mistari miwili, kila tuta. Kwa nafasi hii kiasi cha kil 60-75 za mbegu hutumika kwa hekta moja.

Kwa karanga zilizopo kwenye kundi la Spanish/Valencia (zisizotambaa), nafasi kati ya mistari ni sentimita 50, na kati ya mimea ni sentimita 10. Endapo karanga zimepandwa kwenye matuta ya sentimita 90, panda mistari miwili , inayofanya nafasi sawa na sentimita 50 kwa sentimita 10. Kiasi cha kilo 80-100 za mbegu hutumika kwa hekta moja kwa kutumia nafasi hii.Kwa ina zote za mbegu, panda mbegu moja safi, katika kila shimo.

MBOLEA
Kufuatana na majaribio yaliyofanyika imeonekana kuwa karanga hustawi vizuri chini ya viwango vidogo vya phosphorus (TSP, SSP). Vile vile katika sehemu nyingine, karanga zimefanya vizuri kwa kutumia samadi. Ubadilishaji wa mazao (Crop Rotation) husaidia kutunza rutuba, hivyo kupunguza kiasi cha mbolea kinachotumika.Karanga zinaweza kulimwa baada ya mahindi, ili kutumia masalia ya mbolea.

UPALILIAJI
Karanga zipaliliwe zikiwa changa. Shamba lililotayarishwa vizuri na kuondolewa magugu ya muda mrefu (Perrenial weeds) linaweza kupalliwa mara moja, kwa sababu karanga hukua haraka, na zinaweza kushindana na magugu. Baada ya kutoa maua, karanga zisipaliliwe, hii inaweza kuharibu 'pegs', hatimaye kupunguza mavuno.

MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU:
1. MAGONJWA

(i) Ugonjwa wa kuoza (Aflatoxin)
Katika hali ya unyevu mwingi vimelea viitwavyo Aspegilus flavus huota ndani ya maganda na kushambulia mbegu za karanga. Vimelea hivyo hutoa kemikali ambayo ni sumu.

KUZUIAØ Hakikisha kuwa karanga haziharibiwi wakati wa kuchimba.Ø Hakikisha karanga zinakaushwa vizuri (Unyevu wa 10%) kabla ya kuzitunza zitumike kama mbeguØ Karanga za kupanda zitiwe dawa aina ya Fernasan-D.

(ii) Ugonjwa wa Madoa na Kutu: (Cercospora Leaf Spots and Rust)
Magonjwa haya husababisha madoa ya rangi ya kikahawia hadi meusi kwenye majani.
Vimelea vinavyosababisha magonjwa haya viko vya aina tatu:


(a) Cersospora arachidicola. Husababisha Early Leaf Spot.
(b) Phaeoisariopsis personata. Husababisha Late Leaf spot.

Ugonjwa wa Early Leaf Spot hutangulia kuonekana, lakini magonjwa yote mawili yanaweza kujitokeza shambani kuanzia wiki 3-5 baada ya karanga kupandwa.

(c) Puccinia arachidis. Husababisha ugonjwa wa Kutu. 

Kuzuia:Ø Kupanda mapema.Ø Kuondoa maotea ya karanga wakati wa kiangazi.Ø Tumia dawa aina ya Chlorothalonil (Daconil 2787)

Dawa huwekwa kiasi cha kilo l.6 katika lita 800 za maji kwa hekta moja, kila baada ya siku saba, kwa majuma machache kuanzaia maratu dalili za ugonjwa zinapoonekana.
Uchunguzi juu ya aina zinazostahimili magonjwa haya bado unaendele kufanywa kwenye kituo cha utafiti wa kilimo Naliendele.



(iii) Ugonjwa wa Rosette (Rosette virus disease)
Ugonjwa huu huambukizwa na wadudu waitwao "Mafuta" Aphids (Aphis craccivora). Mimea ambayo imeshambuliwa na ugonjwa huu hudumaa, na inakuwa na madoa ya njano.
Ugonjwa wa Rosette (Ukoma)


Kuzuia:Ø Kupanda mapemaØ Panda karanga zako shambani katika nafasi za karibu karibu.Ø Palilia na toa maotea shambani mwako.

(iv) Ugonjwa wa maganda matupu (Empty pods or pops)
Karanga zilizoshambaliwa na ugonjwa huu, huwa lazina mbegu (maganda matupu). Ugonjwa huu husababishwa na ukosefu wa madini ya Calcium (chokaa) kwenye udongo.


Kuzuia:
Tumia Calcium katika hali ya Gypsum (Ca SO4) kwenye mimea au weka Chokaa (lime - CaO)kwenye udongo kabla ya kupanda. Ugonjwa huu uko kwenye mikoa ya kusini mwa Tanzania (Lindi, Mtwara na Ruvuma) na hushambulia sana karanga za muda mrefu kama vile Red Mwitunde.
Majaribio hapa Tanzaniia hayajathibitisha kuweka chokaa (Liming) kuwa ni jibu sahihi la kupambana na ugonjwa huu, lakini ili kupunguza, kupanda mapema ni muhimu.

2. WADUDU WAHARIBIFU

(i) Mafuta Aphids au "Mafuta" (Aphis cracivora) 
Hushambulia karanga kila msimu, lakini athari yao kubwa ni kueneza ugonjwa wa Rosette. Wakati wa mvua nyingi huoshwa toka kwenye majani, hivyo hawaleti madhara.

Kuzuia:
• Kupanda mapema
• kupanda karanga karibu karibu

(ii) Groundnut hopper: Hilda patruelis
Hufyonza mizizi, "pegs", na karanga changa, hivyo husababisha majani kuwa manjano, kunyauka, na mmea kukauka ungali mchanga. Wadudu hawa hushambulia mazao mengine kama vile maharage, kunde. alizeti na korosho, hivyo kunahitajika mzunguko (rotation) mzuri wa mazao.

Kuzuia:
• Kwenye mashamba makubwa, inashauriwa kutumia dawa aina ya Aldrin au chloropyrifos, kuchanganya kwenye ardhi kabla ya kupanda.
• Kunyunyizia Dimethoate mara tu wadudu wanapoonekana.
• Kutochanganya na zao la korosho au mbaazi kwenye shamba moja na karanga.

(iii) Mchwa.
Kuna aina mbili za mchwa ambao hushambulia na kusababisha uharibifu kwenye zao la karanga.
Aina ya kwanza ni wale ambao hutoboa sehemu ya chini kwenye mzizi, au kutengeneza matundu, na hukaa kwenye mmea wa karanga wakati wote zikiwa shambani.
Aina ya pili ni wale ambao hukata matawi yanayokua au kutambaa. Uharibifu huu huonekana zaidi kwenye shamba jipya. Kuchelewa kuvuna kunaweza kusababisha kupotea kwa mazao mengi, kutokana na kuharibika kwa mizizi, na kusababisha karanga nyingi kubakia shambani wakati wa kuvuna.

Kuzuia:
Mchwa wanaweza kuzuiwa kwa kutumia dawa aina ya Alandrin 40% ya unga, kwa kiasi cha kilo 2.5 kwa hekta., Njia rahisi ni kuchanganya dawa na mbolea aina ya Phosphate (TSP au SSP) au mchanga na kumwaga shambani kabla ya kupanda karanga.

(iv) Panya:
Hushambulia sana karanga zinapoanza kuota, na wakati zinapokaribia kuvunwa.


Namna ya Kuzuia panya:
• Tumia dawa za kuua panya
• Mitego
• Kuwachimbua toka aridhini walikojificha.
(v) Ndege
Kama panya, ndege hasa kunguru hushambulia sana karanga kabla hazijaota (mara baada ya kupanda), zinapoanza kuota, zinapokaribia na wakati zimekwisha komaa.
s

Kuzuia
• Kutumia mitego
• Kuamia
• Kuweka (kutundika/kuning’iniza) mzoga au kunguru mzima shambani.

UBANGUAJI NA UTUNZAJI WA KARANGA
Kubangua karanga ni kazi ngumu. Mtu mmoja anaweza kubangua kiasi cha kilo 12-15 kwa siku. Karanga zilizopo kwenye kundi la Virginia hubangulika kirahisi, kuliko aina ya Spanish au Valencia. Mashine za kubangulia karanga hupatikana hapa nchini, zinarahisisha kazi, lakini tahadhari isipochukuliwa huharibu karanga.
Karanga zinazokusudiwa kutunzwa kwa muda mrefu, zitunzwe na maganda yake kwenye ghala. Ghala iwe kavu, yenye kupitisha hewa, na imara kuzuia wanyama waharibifu kama vile panya.Ubora na uwezo wa karanga kuota huanza kupotea mara baada ya kubanguliwa.

UJENZI WA BANDA LA KUKU

Ujenzi wa mabanda bora ya kuku ni miongoni mwa mambo ya msingi kabisa katika ufugaji bora wa kuku wawe ni wa asili au wale walioboreshw...